Othman Ash Shaham na Farqad As-Sabakhi walimuuliza Muslim mtoto wa Swahaba mtukufu Abuubakra radhi za Allah ziwe juu yake: Je alisikia kutoka kwa baba yake hadithi kutoka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika fitina na vita itakayotokea baina ya waislamu? Akasema: Naam, alieleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake ya kwamba itatokea fitina baada ya kifo chake, na fitina hii aliyekaa na kughafilika nayo ni bora kuliko anayetembea ndani yake, na anaitafuta pasina kujua, na anayetembea ndani yake ni bora kuliko anayekwenda mbio kuiendea na kuitafuta na kushiriki ndani yake. Kisha akaelekeza Mtume rehema na amani ziwe juu yake itakayeshuka na kufika fitina katika zama zake na kwake kukapatikana upenyo atakaokimbilia; atakayekuwa na ngamia anayechunga basi aifuate ngamia yake, na atakayekuwa na mbuzi anayechunga basi amfuate mbuzi wake, na atakayekuwa na ardhi na shamba basi aende shambani kwake. Bwana mmoja akasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu hivi wasemaje kwa mtu ambaye hatokuwa na makimbilio kama ngamia wala mbuzi wala shamba? Akasema: Basi aende akachukue silaha yake aipige na ailainishe, kisha akimbie na ajinusuru yeye na mwanaye ikiwa ataweza kuokoka. Kisha akataka ushuhuda rehema na amani ziwe juu yake mara tatu, akasema: Ewe Allah je, nimefikisha? Ewe Allah je nimefikisha? Ewe Allah je nimefikisha?. Bwana mmoja akasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu wasemaje ikiwa nitalazimishwa kushiriki pamoja na safu moja, au moja kati ya makundi mawili, akanipiga mtu kwa panga lake, au mshale ukanilenga ukaniuwa?. Akasema: Atarudi na madhambi yake na madhambi ya aliyemuuwa, na siku ya Kiyama atakuwa miongoni mwa watu wa motoni.