Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuhusu Mwenyezi Mungu kunong'ona na mja wake muumini siku ya Kiyama, akasema: Atasogezwa muumini siku ya Kiyama karibu na Mola wake Mlezi kisha atamuwekea pazia lake la kumkinga na watu walioko katika kisimamo, hakuna atakayeona katika pazia hilo zaidi yake, hapo atamwambia: Je walijua dhambi fulani na fulani... atamtaka akiri madhambi yake yaliyokuwa kati ya mja na Mola wake Mlezi. Naye atasema: Ndiyo, ewe Mola Mlezi. Mpaka atakapofadhaika muumini na kuogopa, Mtukufu atamwambia: Mimi niliyasitiri kwako madhambi haya duniani, na mimi leo hii ninayasamehe kwa ajili yako, hapo atapewa faili la mema yake. Na ama kafiri na mnafiki wataitwa mbele ya kadamnasi: Hawa ndiyo waliomkadhibisha Mola wao Mlezi, basi tambueni kuwa laana za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya madhalimu.