Mtu mmoja miongoni mwa watu wa Najdi alikuja kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake na nywele zake zikiwa zimetimkatimka na sauti yake ikiwa juu, wala haeleweki anasema nini, mpaka alipomkaribia Mtume rehema na amani ziwe juu yake akauliza kuhusu faradhi za Uislamu? Basi Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, akaanza na swala, na akamwambia kuwa Mwenyezi Mungu amemfaradhishia kuswali swala tano katika kila mchana na usiku. Akasema: Je, ninalazimika kuswali swala zingine zaidi ya hizi tano? Akasema: Hapana, labda kama utajitolea kuswali swala za sunna. Kisha akasema rehema na amani ziwe juu yake: Na miongoni mwa ibada alizokuwajibishia Mwenyezi Mungu juu yako ni kufunga mwezi wa Ramadhani. Yule bwana akasema: Je, ninalazimika kufunga funga zingine zaidi ya swaumu ya Ramadhani? Akasema: Hapana, ila kama utajitolea kufunga. Kisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake akamtajia Zaka Yule bwana akasema: Je, ninalazimika chochote katika sadaka baada ya zaka ya faradhi? Akasema: Hapana, ila kama utajitolea. Baada ya mtu huyo kusikia faradhi hizo kutoka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake aligeuka na kuapa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa atashikamana nazo bila ya kuongeza wala kupunguza, akasema rehema na amani zimshukie baada ya kauli yake hiyo: Ikiwa bwana huyu atakuwa mkweli kwa alichoapia, basi atakuwa miongoni mwa waliofaulu.