Ameeleza Raafi bin Khadiji radhi za Allah ziwe juu yake ya kwamba wao walikuwa pamoja na Mtume rehema na amani ziwe juu yake eneo la Dhul-Hulaifa, watu wakapatwa na njaa, na walikuwa wamepata ngawira kutoka kwa washirikina, ngamia pamoja na mbuzi, wakafanya haraka kabla ngawira hazijagawanywa wakazichinja, na wakabandika vyungu jikoni, pasina ya kumuomba idhini Mtume rehema na amani ziwe juu yake, na alikuwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake akitembea mwishoni mwa watu, alipojua hilo Mtume rehema na amani ziwe juu yake aliamrisha vyungu vikamiminwa pamoja na mchuzi wake, kisha akawagawia ngawira baina yao, akafanya mbuzi kumi ni sawa na ngamia mmoja, ngamia mmoja katika hao akakimbia, wakashindwa kumkamata wala kumpata, na farasi walikuwa wachache, bwana mmoja akampiga yule ngamia kwa mshale, Mwenyezi Mungu akawazuilia, akasema rehema na amani ziwe juu yake: Hakika wanyama hawa wafugwao wana tabia kama tabia za wanyama pori, watakapokushindeni miongoni mwao na hamkuweza kuwakamata basi fanyeni hivyo. Akasema Raafi: Hakika sisi tunataraji kukutana na maadui zetu kesho na tunahofia kuharibu makali ya silaha zetu ikiwa tutazichinjia, na tunahaja kubwa ya kuchinja, na hatuna kisu, je tuchinje kwa miti ya mwanzi mikavu? Akasema rehema na amani ziwe juu yake: Kitakachomwaga damu na kikaitiririsha na kikaimwaga kwa wingi, na likatajwa jina la Mwenyezi Mungu, basi kuleni, isipokuwa jino na kwato, na nitakuhadithieni kuhusu hilo: Ama jino ni mfupa, na ama kwato hizo makafiri wa Ethiopia huzitumia.