Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Hadithil Qudsi (tukufu): Ewe mwanadam, madam unaniomba na kutaraji rehema yangu, wala hujakata tamaa; Nitayasitiri madhambi yako na kuyafuta, bila kujali, hata kama madhambi na maasi haya ni katika madhambi makubwa. Ewe mwanadam! Lau madhambi yako yangekuwa mengi sana kiasi cha kuijaza nafasi ya baina ya mbingu na ardhi mpaka kiasi cha kufikia upenyo wake na kufunika pembe zake, kisha ukaniomba msamaha, basi ningekufutia na kukusamehe madhambi yote, bila kujali wingi wake. Ewe mwanadam: Lau ungenijia mimi baada ya kufa ukiwa na madhambi na maasi ujazo wa ardhi, na ukafa haliyakuwa unanipwekesha hukunishirikisha na chochote; Ningekutana na madhambi na maasi haya nikiijaza ardhi kwa msamaha; kwa sababu mimi ni mwingi wa msamaha, na ninasamehe madhambi yote isipokuwa shirki.