Siku moja alisali Mtume rehema na amani ziwe juu yake swala ya Alfajiri, kisha akauliza: Je, fulani kahudhuria nasi swala yetu hii? Maswahaba wakasema: Hapana. Kisha akasema: Hivi fulani kahudhuria? kwa mtu mwingine, wakasema: Hapana. Akasema rehema na amani ziwe juu yake: Hakika swala ya Alfajiri na Ishaa ni swala nzito kwa wanafiki; kwa sababu ya kuzidi kwa uvivu katika nyakati hizi, na ni kwa sababu ya uchache wa kutoonekana kwa watu, kwa sababu gizani hawaonekani. Na lau kama mngejua enyi waumini yaliyomo ndani ya swala hizi mbili Alfajiri na Ishaa katika malipo na thawabu za ziada, kwa sababu malipo huwa kwa kadiri ya tabu, basi mgeziendea hata kwa kutambaa na kwa kutembea kwa mikono na magoti. Na hakika safu ya kwanza katika ukaribu wake na imam ni kama safu za Malaika ukaribu wake na Mwenyezi Mungu Mtukufu, na lau waumini wangelijua ni zipi fadhila za safu ya kwanza basi wangeshindana kuiwahi, Hakika swala ya mtu na mtu mwingine inamalipo makubwa na ina athari kubwa kuliko swala yake peke yake, na swala yake pamoja na watu wawili ni bora kuliko swala yake na mtu mmoja, Na swala ambayo waswaliji watakuwa wengi hiyo ndio swala bora inayopendeka kwa Mwenyezi Mungu.