Ameeleza Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- kuwa hakuna mja yeyote atakayetenda dhambi, akatawadha vizuri, kisha akasimama na akaswali rakaa mbili kwa nia ya kuomba toba kutokana na dhambi lake hili, kisha akamuomba Allah msamaha, isipokuwa Mwenyezi Mungu humsamehe. Kisha Mtume -Rehema na amani ziwe juu yake- akasoma kauli yake Mtukufu: "Na wale ambao wakitenda dhambi kubwa au wakizidhulumu nafsi zao kwa kutenda dhambi chini ya hizo, wanaikumbuka ahadi ya Mwenyezi Mungu ya malipo mema kwa wanaomtii na malipo mabaya kwa wanaomuasi na wanaelekea kwa Mola wao hali ya kutubia wakawa wanamuomba Awasamehe madhambi yao na wakawa wana yakini kwamba hapana anayesamehe madhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na wao kwa sababu hiyo hawaendelei kwenye maasi, na wao wanajua kwamba wakitubia Mwenyezi Mungu Atawakubalia toba yao". [Surat Al-Imran: 135].