Alitoka Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika siku ya Iddi kwenda katika uwanja wa swala, na alikuwa kawaahidi wanawake kuwa atawatengea nafasi ya kuwapa mawaidha, akaitimiza siku hizo, na akasema: Enyi kundi la wanawake toeni sadaka, na zidishe kuomba msamaha; kwani mambo mawili hayo ni katika sababu kubwa za kufutiwa madhambi, kwani mimi nilikuoneni usiku niliopandishwa mbinguni mkiwa wengi motoni. Mwanamke mmoja miongoni mwao mwenye akili na mawazo mazuri na heshima, akasema: Kwani tuna nini sisi ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu mpaka tuwe wengi motoni? Akasema: Kwa sababu ya mambo kadhaa: Mnazidisha sana kulaani na matusi, na mnakanusha haki za waume. Kisha akawasifu kwa kauli yake rehema na amani ziwe juu yake: Sijapata kuona wenye mapungufu ya akili na dini wanaoweza kuwashinda wenye mioyo salama na akili na maamuzi na uwezo wa kutunza kumbukumbu zao kuliko nyinyi. Akasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na ni upi upungufu wa akili na dini? Akasema: Ama upungufu wa akili ni kuwa ushahidi wa wanawake wawili unalingana na ushahidi wa mwanaume mmoja; huu ndio upungufu wa akili, na upungufu wa dini, ni upungufu wa kufanya amali njema, kiasi ambacho mwanamke anakaa siku kadhaa haswali kwa sababu ya hedhi, na anafungua siku kadhaa za Ramadhani kwa sababu ya hedhi, na huu ndio upungufu wa dini, isipokuwa wao hawalaumiwi wala hawaandikiwi dhambi juu ya hilo; kwa sababu ni katika asili ya maumbile, kama ambavyo mwanadamu ameumbwa na asili ya kuipenda mali, na haraka katika mambo yake na ni mjinga.... na mengineyo, lakini alilitanabahisha hilo ikiwa ni tahadhari kwa wanaume wasifitinike nao.