Alikuwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake katika kundi la Masahaba, akawataka mara tatu mfululizo wampe ahadi ya utiifu na wampe ahadi ya kushikamana na mambo haya: La kwanza: Kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake kwa kutekeleza amri zake na kujiepusha na makatazo yake, na wasimshirikishe na kitu kingine. La pili: Kusimamisha swala tano za faradhi, katika usiku na mchana. La tatu: Kusikia na kutii katika mambo mema kwa yule atakayesimamia majukumu ya waislamu. La nne: Kushusha haja zao zote kwa Mwenyezi Mungu na wasiwaombe watu chochote katika haja hizo, na katika hilo Mtume rehema na amani ziwe juu yake akashusha sauti yake. Na hakika Masahaba radhi za Allah ziwe juu yao waliyafanyia kazi yale waliyoyatolea ahadi, mpaka akasema mpokezi wa hadithi: Hakika niliwaona baadhi yao hao Masahaba unadondoka mjeledi wa mmoja wao, na hamuombi yeyote amuokotee, bali anashuka na anauchukua yeye mwenyewe.