Alikaa Mtume rehema na amani ziwe juu yake siku moja juu Mimbari akiwahadithia Maswahaba zake akasema: Hakika kikubwa ninachokihofia zaidi kwenu nyinyi baada yangu ni yale mtakayofunguliwa katika baraka za Ardhi na maua ya Dunia na pambo lake, na muonekano wake, na yale yaliyomo miongoni mwa aina mbalimbali za starehe na nguo na mazao na mengineyo miongoni mwa yale ambayo watu hujifaharisha kutokana na uzuri wake pamoja nakuwa yanadumu kwa muda mchache. Mtu mmoja akasema: Maua ya Dunia ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, je inaweza kurudi neema hii na kuwa janga na adhabu?! Watu wakamlaumu muulizaji pale walipomuona Mtume rehema na amani ziwe juu yake kanyamaza, na wakadhania kuwa kamkasirisha. Ikabainika kuwa rehema na amani ziwe juu yake alikuwa akiteremshiwa wahyi, kisha akaanza kufuta jasho katika paji lake la uso, akasema: Yuko wapi muulizaji? Akasema: Mimi. Akamhimidi Mwenyezi Mungu na akamsifia, kisha akasema rehema na amani ziwe juu yake: Kheri ya kweli haiji ila kwa kheri, lakini maua haya si kheri halisi kwa kuwa yanapelekea katika fitina na kushindana na kushughulika nayo na kuwacha kuielekea Akhera kikamilifu, kisha akapigia mfano wa hilo akasema: Hakika mimea ya masika na kijani chake; nayo ni aina za mimea ambazo huwapendeza sana wanyama, na huwaua kwa kuila kwa wingi na kuvimbewa au hukaribia kuwaua, isipokuwa mnyama anayekula mimea ya kijani aliyekula mpaka ikajaa sehemu ya tumbo lake, akaelekea juani na akatoa kinyesi chepesi kutoka tumboni mwake au akakojoa, kisha akayacheua yaliyoko tumboni mwake kisha akayatafuna kisha akayameza, kisha akarudi kula tena. Hivyo mali hii ni kama majani ya kijani matamu, yanaua au yanakaribia kuuwa yanapokithiri; isipokuwa kama atatosheka na kidogo ambacho anahaja nacho na kitakachomtosha kwa njia ya halali, hii haidhuru, na neema bora ya muislamu ni kwa yule atakayetoa na kumpa masikini na yatima na mpitanjia, na yule mwenye kuichukua kwa haki atakabarikiwa katika mali hiyo, na atakayeichukua pasina haki yake mfano wake ni kama mfano wa yule anayekula wala hashibi, na mali hiyo itakuwa shahidi juu yake siku ya Kiyama.