Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa Mwenyezi Mungu amempa mambo matano ambayo hakupewa yeyote katika Manabiii kabla yake: La kwanza: Nimeepushwa na hofu, na hofu hiyo inatiwa katika nyoyo za maadui zangu hata kukiwa kati yangu na wao mwendo wa kutembea mwezi mzima. La pili: Tumefanyiwa Ardhi kwetu kuwa Msikiti tuswali mahala popote tutakapokuwa, na udongo wake ni twahara (safi) pale tunaposhindwa kutumia maji. La tatu: Tumehalalishiwa ngawira za vita, nazo ni zile wanazozichukua waislamu katika vita vyao na makafiri. La nne: Nimepewa utetezi mkubwa katika kuwapumzisha watu na misukosuko ya kisimamo cha siku ya Kiyama. La tano: Nimetumwa kuja kwa viumbe wote binadam wao na majini wao, kinyume na Manabii walikokuwa kabla yake, walikuwa wakitumwa kwa watu wao pekee.