Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuhusu aina tatu za watu, wenye kustahiki adhabu ya Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama kwa adhabu tatu, endapo hawatotubia au kusamehewa adhabu: Ya kwanza: Hatowasemesha Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama kwa sababu ya ukali wa ghadhabu yake, bali atawapuuza, au atawasemesha maneno yasiyowafurahisha na yanayoonyesha hasira yake juu yao. Ya pili: Hatowatakasa wala hatowasifia wala hatowasafisha kutokana na madhambi. Ya tatu: Watakuwa na adhabu yenye kuumiza sana Akhera. Na watu wa aina hiyo ni: Aina ya kwanza: Mtu mzima na anajiingiza katika machafu ya zinaa. Ya pili: Fakiri asiyekuwa na mali lakini pamoja na hivyo ana kiburi kwa watu. Ya tatu: Anayekithirisha kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu katika kuuza na kununua, analidhalilisha jina la Mwenyezi Mungu, na analifanya kuwa ndio nyenzo ya kujipatia mali.