Amebainisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa miongoni mwa haki za muislamu juu ya ndugu yake muislamu ni mambo sita: La kwanza: Amsalimie akikutana naye kwa kusema: Assalaam alaikum, naye atajibu salamu kwa kusema: Waalaikumussalaam. La pili: Kuitika wito wake atakapomuita kwa ajili ya sherehe ya harusi au nyingineyo. La tatu: Kumpa nasaha akizihitajia, na wala usimsifie bure, au kumfanyia udanganyifu. La nne: Akipiga chafya akasema: Alhamdulillaah, basi muombee dua kwa kusema: Yar-hamkallaah (Akuhurumie Mwenyezi Mungu), naye ajibu kwa kusema: Yah-diikumullaahu wayuslih baalakum (Akuongozeni Mwenyezi Mungu na kutengenezeeni hali zenu). La tano: Akamuone na amtembelee atakapougua. La sita: Amswalie atakapofariki, na alisindikize jeneza lake mpaka azikwe.