Ameeleza Mama wa waumini Aisha radhi za Allah ziwe juu yake sehemu ya swala ya Mtume rehema na amani ziwe juu yake yakwamba alikuwa akifungua swala yake kwa takbira ya kufungua swala, akisema: "Allaahu Akbaru", na akifungua kisomo kwa suratul Faatiha. "Alhamdulillaah Rabbil A''alamiin..." Na alikuwa anaporukuu baada ya kisimamo, hainui kichwa chake na wala hakishushi wakati wa rukuu, bali anakifanya kilingane sawa kikiwa kimenyooka, na akinyanyua kichwa chake kutoka katika rukuu ananyooka wima kabla hajasujudu, na akinyanyua kichwa chake kutoka katika sijida ya kwanza, hasujudu sijida ya pili mpaka atuliazane akiwa amekaa. Na alikuwa akikaa baada ya kila rakaa mbili kwa ajili ya tahiyatu, na anasema: "Attahiyyatu lillaahi was swalawaatu wat twayyibaatu...", na alikuwa anapokaa baina ya sijida mbili au kwa ajili ya tahiyatu analaza mguu wake wa kushoto na kuukalia, na anasimamisha mguu wake wa kulia. Na anamkataza mwenye kuswali kukaa ndani ya swala yake kama mkao wa Shetani, nao ni kulaza miguu yake yote miwili katika Ardhi, na kukaa kwa pande zake mbili za nyuma, au kuambatanisha makalio yake na Ardhi na akasimamisha miguu yake na kuweka mikono yake katika Ardhi kama anavyoitandaza mbwa, au akalaza mwenye kuswali mikono yake kwa kuinyoosha katika sijida kama anavyoilaza mnyama mkali. Na alikuwa akihitimisha swala yake kwa salamu: "Assalaam alaikum warahmatullah" upande wa kulia mara moja na mara nyingine upande wa kushoto.