Alikuwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake msikitini kwake akiwa pamoja na Maswahaba zake, akaja bedui mmoja kutoka kijijini, akaanza kukojoa katika kona ya msikiti. Maswahaba wakamkaripia na wakasema: Koma, na wacha unachokifanya. Akasema rehema na amani ziwe juu yake: Muacheni, na wala msimkatishe mkojo wake, wakamuacha mpaka akamaliza. Kisha rehema na amani ziwe juu yake akamuita na akamwambia: Hakika misikiti haifai kwa chochote miongoni mwa mikojo hii, wala aina yoyote ya uchafu, bali ni kwa ajili ya kumtaja Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka, na swala, na kusoma Qur'ani na mfano wa hayo. Kisha akamuamrisha rehema na amani ziwe juu yake mtu mmoja katika Maswahaba akaja na ndoo iliyojaa maji akayamwaga katika mkojo wake.