Lilikuja kundi la Maswahaba radhi za Allah ziwe juu yao, katika nyumba za wake za Mtume rehema na amani ziwe juu yake, wakiuliza kuhusu ibada zake za siri ndani ya nyumba yake, walipoelezwa wakawa kana kwamba za kwao wameziona ndogo, wakasema: Na tuko wapi sisi na Mtume rehema na amani ziwe juu yake? hali yakuwa amekwisha samehewa yaliyotangulia katika madhambi yake na yajayo, ukilinganisha na ambaye hajajua hata kupatikana kwa msamaha, huyu anahitaji kupitiliza katika kufanya ibada huenda akaupata msamaha huo. Kisha wakasema baadhi yao: Sitooa wanawake. Na wakasema baadhi yao: Sitokula nyama. Na wakasema baadhi yao: Sitolala katika godoro. Hilo likamfikia Mtume rehema na amani ziwe juu yake, akachukia, na akawahutubia watu, akamhimidi Mwenyezi Mungu na akamtukuza, na akasema: Wana nini watu fulani waliosema kadhaa wa kadhaa?! Wallahi mimi ndiye ninayemuhofu sana Mwenyezi Mungu kuliko watu wote na ndiyo mchamungu wenu, lakini ninalala ili nipate nguvu ya kusimama, na ninafungua ili nipate nguvu ya kufunga, na ninaoa wanawake, atakayeipuuza njia yangu, na akaona njia nyingine ndio iliyokamilika, na akachukua njia ya asiyekuwa mimi, huyu hayuko nami.