Mtume rehema na amani ziwe juu yake alikuwa safarini katika vita na akiwa pamoja na Maswahaba zake miongoni mwa Muhajirina na Maanswari radhi za Allah ziwe juu yao, mtu mmoja katika Muhajirina akampiga mgongoni mtu mmoja miongoni mwa Maanswari kwa mkono wake. Answari akasema: Nipeni msaada enyi Maanswari, na akasema Muhajiri: Nipeni msaada enyi Muhajirina, akawasikia Mtume rehema na amani ziwe juu yake, akasema: Nini hiki?. Wakasema: Mtu mmoja katika Muhajirina kampiga mtu katika Maanswari kwa mkono wake, Answari akasema: Nipeni msaada enyi Maanswari, na Muhajiri akasema: Nipeni msaada enyi Muhajirina. Akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Achaneni na desturi hii ya kijinga, kwani ni mbaya inachukiza na ina udhi; nayo ni kwamba mtu akizidiwa na mgomvi wake anawaita watu wake wanaanza kumsaidia sawa sawa awe kadhulumu au kadhulumiwa, kwa sababu ya ujinga wao, na ubaguzi wao. Amesema Jabiri: Na Maanswari wakati amefika Mtume rehema na amani ziwe juu yake mji wa Madina walikuwa wengi, kisha Muhajirina wakawa wengi baada ya hapo. Akasema kiongozi wa unafiki Abdallah bin Ubai bin Saluli: Jambo limefikia huko?! Wallah tukirejea Madina watukufu (anajikusudia yeye na watu wake) watawatoa katika mji wa Madina madhalili (anakusudia Mtume rehema na amani ziwe juu yake na watu wake). Akasema Omari bin Khattwab radhi za Allah ziwe juu yake: Hebu, niache ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nikate shingo ya huyu mnafiki, akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Muache, ili watu wasiseme kuwa Muhammadi anauwa wafuasi wake, hata kama ni kwa dhahiri.