Amekataza Mtume rehema na amani ziwe juu yake mwanaume kutazama uchi wa mwanaume mwenzie, au mwanamke kutazama uchi wa mwanamke mwenzie. Uchi: Ni kila kinachoonewa aibu kinapodhihiri, na uchi wa mwanaume ni kati ya kitovu chake na magoti yake, Na mwanamke mwili wake wote ni uchi kwa mwanamke asiye mume wake au ndugu wa damu, na upande wa wanawake kwa ndugu zao wa damu, anaweza kuonyesha viungo ambavyo kwa desturi ya kawaida huonekana wakati wa kufanya kazi zake za nyumbani. Na amekataza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kukaa faragha mwanaume na mwanaume mwenzake ndani ya nguo moja, au ndani ya kifuniko kimoja wakiwa uchi, na mwanamke kukaa faragha na mwanamke mwenzie ndani ya nguo moja au ndani ya kifuniko kimoja wakiwa uchi; kwa sababu kitendo hicho huenda kikapelekea kila mmoja kugusa uchi wa mwenzie, na kuugusa ni haramu ni kama kuuangalia, bali hilo ni haramu zaidi; kwa sababu linapelekea katika uovu mkubwa.