Walikuja watu kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake, kutoka katika kabila la Ukli na Uraina wakiwa ni Waislamu, wakapatwa na ugonjwa na maradhi mazito kwao, yakavimba matumbo yao, wakachukia kuishi Madina kwa sababu chakula hakikuwapendeza wala hali ya hewa. Mtume rehema na amani ziwe juu yake akawaamuru waende katika ngamia za sadaka, na wanywe mikojo na maziwa yake. Wakaenda, na walipopona, na wakanenepa, na rangi zao zikarejea kuwa nzuri, wakamuua mchungaji wa ngamia wa Mtume rehema na amani ziwe juu yake, na wakachukua ngamia. Habari hiyo ilifika asubuhi na mapema, ndipo Mtume akatuma kikosi cha kuwafuata. Wakawakamata, wakati wa jua kupanda juu wakaletwa wakiwa mateka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake. Mtume akaamuru mikono yao na miguu yao ikatwe, na macho yao yakatobolewa, kwa sababu walimtendea hivyo mchungaji. Kisha wakatupwa kwenye eneo lenye joto (al-Harra), wakawa wakiwaomba maji lakini hawakupewa mpaka walipokufa. Amesema Abuu Qilaba: Ni kwamba wao waliiba, na wakaua, na wakakufuru baada ya imani yao, na wakampiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake.