Alikuja mtu mmoja katika Mayahudi kwa kiongozi wa waumini Omari radhi za Allah ziwe juu yake akasema kumwambia: Kuna aya ndani ya kitabu chenu cha Qur'ani mnaisoma, lau ingeliteremka kwetu jamii ya Mayahudi katika kitabu chetu cha Taurati basi tungeifanya siku hiyo kuwa sikukuu kwa kuisherehekea; kwa kushukuru neema ya kuteremka aya hii tukufu, Omari radhi za Allah ziwe juu yake akasema kumwambia: Ni Aya ipi?. Akasema: "Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini." Akasema Omari radhi za Allah ziwe juu yake: Tunaijua siku hiyo, na sehemu iliyoteremka aya hii tukufu, aya hiyo imeteremka siku ya Iddi, nayo ni siku ya Ijumaa kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake naye akiwa amesimama Arafa, nazo ni siku mbili tukufu kwa Waislamu.