Ameeleza mama wa Waumini, Aisha, Allah amuwiye radhi, kwamba jambo la kwanza aliloanziwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake ni njozi za kweli usingizini, akawa haoti kitu katika njozi zake isipokuwa kilitokea wazi mfano wa nuru ya asubuhi, kisha akapendezeshwa kujitenga, na alikuwa akijitenga ndani ya pango la Hiraa akifanya ibada kwa siku kadhaa, kabla ya kurudi katika familia yake, na alikuwa akichukua chakula cha kumtosheleza, kisha anarejea kwa mama wa waumini Khadija radhi za Allah ziwe juu yake, anachukua tena chakula cha kutosha idadi ya siku kama hizo, mpaka ikamjia amri ya kweli, naye akiwa katika pango la Hira. Kisha akamjia Malaika Jibril amani iwe juu yake, akamwambia: Soma, akasema rehema na amani ziwe juu yake: Mimi si mzuri katika kusoma, anasema: Akanishika akanibana mpaka nikachoka na kuishiwa nguvu, kisha akaniachia na kusema: Soma. Nikasema: Mimi si mzuri katika kusoma, basi akanichukua na kunibana kwa mara ya pili mpaka nikachoka na kuishiwa nguvu, kisha akaniacha, akasema: Soma. Nikasema: Sijui kusoma, basi akanichukua na akanifunika mara ya tatu, kisha akaniacha na akasema: "Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliyeumba. Kamuumba mwanadamu kutokana na pande la nyama. Soma na Mola wako Mlezi ni Mkarimu" [Al-Qalaq: 1-3]. Akarejea Mtume rehema na amani ziwe juu yake akiwa na aya kadhaa, lakini kifua chake kilikuwa kikitetemeka kwa kuhofia kifo, akaingia kwa mkewe mama wa waumini Khadija binti Khuwailidi radhi za Allah ziwe juu yake akasema: Nifunikeni na nguo, nifunikeni na nguo, wakamfunikwa kwa nguo mpaka hofu ikamuondokea, akasema kumwambia Khadija na akampa habari ya kilichotokea, na akasema: Nilihofia kifo juu ya nafsi, Khadija akasema: Si hivyo, Wallahi hawezi kukufedhehesha Mwenyezi Mungu kamwe! Hakika wewe utaunga udugu, na utamsaidia mnyonge ambaye jambo lake halina muelekeo, na utamnyanyua fakiri asiye na kitu; kiasi ambacho utawapa watu yale wasiyoyapata kwa asiyekuwa wewe, na utamkirimu mgeni, na utasaidia kutatua matatizo ya haki. Khadija akamchukua mpaka akamfikisha kwa Waraqa bin Naufali bin Asadi bin Abdil -Uzza, ambaye ni mtoto wa ami yake, na alikuwa ni mtu aliyeachana na mila za kale na akawa mkristo, na alikuwa akiandika kutoka katika Injili kwa lugha ya Kiebrania kiasi alichokitaka Mwenyezi Mungu akiandike, na alikuwa ni mzee mtu mzima aliyepofuka macho yake, Khadija akasema kumwambia: Ewe mtoto wa ammi, hebu msikilize mtoto wa ndugu yako, Waraqa akasema kumwambia: Ewe mtoto wa ndugu yangu, umeona nini? Mtume rehema na amani ziwe juu yake akamueleza habari ya kile alichokiona, Waraqa akasema kumwambia: Huyo ni Malaika Jibrili aliyemteremsha Mwenyezi Mungu kwa Musa amani iwe juu yake, natamani lau ningekuwa wakati huo ni kijana mwenye nguvu, laiti kama nitakuwa hai, wakati wakikufukuza watu wako, akasema rehema na amani ziwe juu yake: Hivi, kwani wao watanifukuza?!. Akasema: Ndiyo, kamwe hajawahi kuja mtu na mfano wa hiki ulichokujanacho isipokuwa aliudhiwa na kutendewa uadui, na ikiwa siku yako hiyo itanikuta nikiwa hai basi nitakutetea utetezi wa nguvu. Kisha hakukaa muda mrefu Waraqa akawa amefariki, na wahyi ukachelewa kuteremka tena kwa muda kidogo.