Ameeleza Mtume rehema na amani ziwe juu yake kuwa atakayesema: "Hapana Mola" na hakuna muabudiwa wa haki "isipokuwa Mwenyezi Mungu, yeye pekee asiye na mshirika" katika uungu wake na ulezi wake na majina yake na sifa zake, "Ufalme ni wake" na maamuzi na mipangilio yote, "naye juu ya kila kitu ni muweza" pasina wa kumzuia wala wa kumkinga, na asiyoyataka hayawezi kuwa. Atakayesema dhikiri hii kwa siku mara mia moja, ataandikiwa ujira kutoka kwa Mwenyezi Mungu sawa na aliyeacha huru watumwa kumi, na ataandikiwa kwa maneno hayo mema mia moja na daraja Peponi, na yatafutwa kwake makosa mia moja, na yatakuwa ni kinga na kizuizi na ngome dhidi ya Shetani na upotovu wake na usaliti wake katika siku yake hiyo mpaka iingie jioni kwa kuzama jua, na hatoleta yeyote siku ya Kiyama kitu bora kuliko alichokuja nacho, isipokuwa mtu aliyefanya zaidi ya hivyo na akazidisha zaidi ya hapo.