Aliingia bedui mmoja msikiti wa Mtume rehema na amani ziwe juu yake siku ya Ijumaa kupitia mlango wa Magharibi upande wa nyumba ya Omari bin Khattwab radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na Mtume rehema na amani ziwe juu yake akiwa kasimama anahutubia, yule bwana akamuelekea Mtume rehema na amani ziwe juu yake, na akasema, ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, wanyama wameangamia, na njia zote zimekatika kwa kufa mifugo inayobeba watu, au imedhoofika kutokana na njaa, basi muombe Mwenyezi Mungu atunyeshelezee mvua. Akanyanyua rehema na amani ziwe juu yake mikono yake, kisha akasema: Ewe Mwenyezi Mungu tunyeshelezee, Ewe Mwenyezi Mungu tunyeshelezee, Ewe Mwenyezi Mungu tunyeshelezee. Amesema Anasi bin Maliki radhi za Allah ziwe juu yake: Wallahi hatukua tukiona mbinguni hata kipande cha mawingu, na hapakuwa kati yetu sisi msikitini na Mlima Sal'i ulioko Magharibi mwa msikiti upande ambao hujia mawingu nyumba wala makazi yanayoweza kutuzuia kuona mawingu. Amesema Anasi radhi za Allah ziwe juu yake: Likatokeza nyuma yake wingu la duara mfano wa ngao nayo ni mviringo mdogo, lilipofika kati kati ya mawingu ya Madina likatanda, kisha mvua ikaanza kunyesha, na namuapa Mwenyezi Mungu, hatukuliona Jua tena kutokana na mvua mpaka Ijumaa iliyofuata, kiasi kwamba aliingia tena yule bwana kupitia mlango ule ule, huku rehema na amani ziwe juu yake akiwa kasimama anahutubia, akamuelekea akiwa wima, akasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, mali zimeangamia na njia zimekatika, basi muombe Mwenyezi Mungu aizuie mvua kwetu. Akasema: Akanyanyua rehema na amani ziwe juu yake mikono yake, kisha akasema: Ewe Mwenyezi Mungu igeuze mvua iende pembezoni mwetu ewe Mwenyezi Mungu ielekee katika sehemu zenye miinuko katika Ardhi kama kichuguu, na milima midogo, na ndani ya mabonde, na maoteo ya miti. Akasema Anasi: Yakakatika mawingu ya mvua, na tukatoka tukitembea juani.