Amesimulia Abuu Burda radhi za Allah ziwe juu yake kuwa baba yake Abuu Mussa Al-Ash'ary radhi za Allah ziwe juu yake aliugua maradhi makali, akazimia, na kichwa chake kilikuwa katika paja la mwanamke mmoja katika wake zake, akapiga mayowe yule mwanamke kwa kumuita, akawa hakuweza kumjibu chochote kwa sababu ya kuzimia kwake. Alipozinduka akasema kuwa: Hakika yeye anajitenga mbali na yule aliyejitenga mbali naye Mtume rehema na amani ziwe juu yake, na hakika yeye rehema na amani ziwe juu yake alijitenga naye. Mpiga mayowe: Naye ni mwanamke anayenyanyua sauti yake wakati wa msiba. Na mnyoaji: Ni mwanamke anayenyoa nywele zake wakati wa msiba. Na mchana nguo: Ni mwanamke anayechana nguo zake wakati wa msiba. Kwa sababu haya ni katika mambo ya zama za ujinga, bali aliamrisha kuwa na subira wakati wa msiba, na kutaraji malipo yake kwa Mwenyezi Mungu.