Aliwaamrisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake waislamu mambo saba na akawakataza mambo saba; yale aliyowaamrisha ni: La kwanza: Kumtembelea mgonjwa. La pili: Kusindikiza jeneza na kushiriki katika kumswalia na kumzika, na kumuombea dua. La tatu: Kumuombea dua aliyepiga chafya na akamhimidi Mwenyezi Mungu, kwa kumuambia: Yar-hamukallaah (Akuhurumie Mwenyezi Mungu). La nne: Kumuepusha aliyetoa kiapo na kumuamini, yaani ikiwa litaapiwa jambo hali yakuwa unauwezo wa kumuepusha na tuhuma basi fanya hivyo; ili usimpelekee kulipa kafara kwa kiapo chake. La tano: Kumsaidia aliyedhulumiwa, kwa kumtetea na kuyazuia yanayotokea kwake miongoni mwa dhulma, kwa kadiri ya uwezo. La sita: Kumuitikia mwenye kualika katika walima wa chakula, kama walima wa harusi, au akika, au kinginecho. La saba: Kutangaza utoaji wa salamu na kuuneza na kujibu pia. Na aliyoyakataza ni: La kwanza: Kuvaa pete za dhahabu na kujipamba nazo. La pili: Kunywa kwa kutumia vyombo vya fedha. La tatu: Kukaa katika matandiko, nayo ni magodoro ambayo huwekwa juu ya mgongo wa farasi, na juu ya ngamia, yaliyotengenezwa kwa hariri. La nne: Kuvaa nguo iliyotengenezwa kwa katani ikachanganywa na hariri, na huitwa (Qassi). La tano: Kuvaa hariri. La sita: Kuvaa hariri nzito. La saba: Kuvaa dibaji, nayo ni: Aina bora zaidi ya hariri na ghali zaidi.