Ameeleza kiongozi wa waumini Ally bin Abii Twalib radhi za Allah ziwe juu yake ya kwamba, mtakaponisikia ninakuhadithieni kutoka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake basi hakika mimi sifichi wala sibuni, wala sifuniki haki, bali ninaweka wazi, na kuanguka kwangu kutoka juu mbinguni ni rahisi na ni bora sana kwangu kuliko kusimulia jambo la uongo nikasema kuwa limetoka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake, na nikisimulia mambo yalio kati yangu mimi na watu wengine, basi vita ni udanganyifu, hapo ninaweza kusema kwa mafumbo au kubuni au kuficha, kwani nilimsikia Mtume rehema na amani ziwe juu yake akisema: Watatokea katika zama za mwisho vijana wenye umri mdogo, wasiojitambua (madhaifu wa akili) watakuwa wakisema maneno kutoka ndani ya Qur'ani na wakiisoma kwa wingi, watakuwa wakitoka ndani ya Uislamu na wakivuka mipaka yake, kama mshale utokavyo katika upinde, Imani yao haivuki koromeo zao, mahali popote mtakapokutana nao basi wauweni, kwani kuwaua kwao kuna malipo kwa atakayewauwa, siku ya Kiyama.