Alimuusia Mtume rehema na amani ziwe juu yake muislamu kwa ndugu yake muislamu kumtendea mazuri, na akabainisha baadhi ya yale yanayomlazimu katika wajibu na adabu kwao; na miongoni mwa hayo: Wasia wa kwanza: Msihusudiane kwa kutamani baadhi yenu neema za wengine ziwaondokee. Wa pili: Wala msipandishiane, kwa kuzidisha katika bidhaa hali yakuwa hana nia ya kununua; isipokuwa anataka kumnufaisha muuzaji, au kumdhuru mnunuzi. Ya tatu: Msichukiane; nako ni kutaka kuleta madhara, kitu ambacho ni kinyume na mapenzi; isipokuwa kuchukiana kutakapokuwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu; hapo ni wajibu. Ya nne: Msitengane, nako ni kila mmoja miongoni mwenu kumpa mgongo na kisogo ndugu yake, na akampuuza na kumhama. Ya tano: Wasiuze baadhi yenu juu ya biashara ya wengine, kwa mtu kumwambia aliyenunua bidhaa: Nina bidhaa kama hiyo kwa bei nafuu kuliko hiyo, au nina bidhaa bora kuliko hiyo na kwa bei hiyo hiyo. Kisha akausia rehema na amani ziwe juu yake kwa usia wa ujumla, akasema: Na kuweni kama ndugu kwa kuyaacha yaliyotajwa katika makatazo, na kwa kujitolea mapenzi na huruma na upole na kusikilizana na kusaidizana katika mambo ya kheri, ikiwa ni pamoja na kusafisha mioyo na kunasihiana kwa kila hali. Na miongoni mwa mambo yanayojenga udugu huu: Asimdhulumu ndugu yake muislamu na wala asimfanyie uadui. Na wala asiache ndugu yake muislamu akadhulumiwa akamsaliti katika mahali ambapo anaweza kumtetea na akapata haki yake, na akamuondolea dhulma. Na asimdharau na akamuona duni na akamtazama kwa jicho la kumshusha thamani na kumkejeli; na hilo ni matokeo ya kiburi kilichopo ndani ya moyo. Kisha akabainisha Mtume rehema na amani ziwe juu yake mara tatu kuwa ucha Mungu uko moyoni, na atakayekuwa na ucha Mungu ndani ya moyo wake unaopelekea katika tabia njema, na kumuogopa Mwenyezi Mungu na kumchunga, basi hawezi kumdharau muislamu, na yamtosha kwake kuwa na mambo ya shari na tabia chafu kwa kumdharau ndugu yake muislamu; na hilo ni kwa sababu ya kiburi kilichopo moyoni mwake. Kisha akasisitiza rehema na amani ziwe juu yake hayo yaliyopita kuwa kila muislamu kwa muislamu mwenzake ni haramu: Damu yake: Kwa kumfanyia uadui akamuuwa, au chini ya hapo kama kumjeruhi au kumpiga na mfano wake, na vile vile mali yake: Kwa kuichukuwa pasina haki, na vile vile heshima yake: Kwa kumtukana yeye mwenyewe au ukoo wake.