Ameeleza Anasi bin Maaliki radhi za Allah ziwe juu yake ya kwamba ilipoteremka kwa Mtume rehema na amani ziwe juu yake kauli yake Mtukufu: "Hakika sisi tumekufungulia ewe Muhammadi ufunguzi wa wazi wazi (1) Ili akusameheme Mwenyezi Mungu yaliyotangulia katika madhambi yako na yajayo, na akutimizie neema zake, na akuongoe katika njia iliyonyooka (2) Na Mwenyezi Mungu akunusuru nusura yenye nguvu (3) Yeye ndiye aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili wazidi imani juu ya imani yao. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye majeshi ya mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye ujuzi, mwenye hekima (4) Ili awaingize Waumini wanaume na Waumini wanawake katika Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo, na awafutie makosa yao. Na huko ndiko kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi Mungu (5) [Al-Fat-hi: 1-5]. Hili lilikuwa Wakati wa kurejea kwake kutoka Hudaibia, na wakati Maswahaba wakiwa wamegubikwa na huzuni na unyonge, wakiwa wamezuiliwa kutekeleza Umra, kwa sababu ya yale waliyokubaliana katika mkataba, na dhana yao ilikuwa; yote hayo hayana masilahi na Waislamu, na walichinja vichinjwa vyao hapo Hudaibia, akasema Mtume rehema na amani ziwe juu yake: Kwa hakika imeteremshwa juu yangu aya ni aya inayopendeka zaidi kwangu kuliko dunia nzima, kisha akaisoma.